Tuesday , 10th May , 2016

Jeshi la Polisi mkoani Songwe, kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, lipo mbioni kuanzisha oparesheni ya kukamata madereva wa Bodaboda wasio na leseni lengo likiwa ni kukomesha ajali za barabarani.

Baadhi ya Pikipiki zikiwa zimepaki Jijini Mbeya.

Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani mkoani Songwe Inspecta Chabuluma Gama amesema ataanzisha oparesheni hiyo hivi karibuni kutokana na ajali nyingi zinazotokea mkoani hapa kusababishwa na madereva wa bodaboda wasiojua sheria za barabarani.

Inspecta Gama amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya madereva wa pikipiki za abiria (Bodaboda) katika eneo la Mpemba Mji mdogo wa Tunduma yaliyoandaliwa na Chuo cha Future World.

Amesema imeainika kuwepo kwa madereva wa bodaboda wasiotaka kutumia fursa ya kupewa mafunzo huku pia wakiendelea kuwabeza wachache wanaojitokeza kupata mafunzo hayo na kukata leseni.

Amesema oparesheni hiyo itaanza muda si mrefu na wale wote ambao watabainika hawana vyeti au leseni za udereva watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kutokana na kushindwa kutii sheria za usalama barabarani.

Naye mmoja wa wahitimu wa Mafunzo hayo Emmanuel Punte, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kwani alikuwa hajui sheria za barabarani licha ya kwamba alikuwa anaendesha gari na pikipiki.