Monday , 2nd Mar , 2020

Uongozi wa juu wa klabu ya Azam yeyenye maskani yake Chamazi, Mbagala Jijini Dar es Salaam umebomoa safu yake ya uongozi kuelekea mchezo wa ligi kati yake na Simba SC.

Jaffary Idd Magamga

Miongoni mwa viongozi waliopunguzwa ni Afisa Habari wa klabu hiyo, Jaffary Idd Maganga ambaye alihudumu katika nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Akithibitisha taarifa hiyo, mwenyewe Jaffary Idd Maganga amesema hatokuwepo tena katika nafasi yake kwakuwa amepangiwa kazi nyingine, "leo, Machi 2, 2020 rasmi sitakuwa Afisa Habari wa Azam FC, kampuni imenibadilishia majukumu na nitaendelea kuwa mwanafamilia wa Azam FC, naomba ushirikiano uendelee kuwepo kati ya huyo ambaye atakuja kwani sote ni ndugu," amesema.

"Mimi sitakuwepo katika nafasi hii lakini nitaendelea kuhudumu ndani ya Azam, ninaomba yule atakayekuja mumpe ushirikiano. Kama nimewakosea mnisamehe na yule atakayekuja kama mtaona anakwenda tofauti mwambieni ile aende sawa nanyi", ameongeza.

Mwingine aliyeenguliwa katika klabu hiyo ni kocha msaidizi, Idd Nassor Cheche ambaye pia amedumu na klabu hiyo kwa kipindi kirefu na kuwa msaada mkubwa pale ambapo klabu ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha kutokuwa na kocha mkuu.

Azam FC itakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa ligi utakaopigwa Machi 4 katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Simba ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 65 huku Azam FC ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi 48.