Thursday , 19th Dec , 2019

Msanii Christian Bella, amesema kuwa ameishi kwenye muziki wa Tanzania kwa muda wa miaka 13, ambao umemfanya awe maarufu na kutambulika duniani, licha ya kuwa bado hajapata Uraia wa kuishi moja kwa moja hapa nchini.

Msanii wa Muziki hapa nchini, Christian Bella.

Christian Bella amesema hayo mbele ya waandishi wa habari, wakati anatambulisha Audio na Video ya wimbo mpya, alioufanya na Ali Kiba uitwao Chaku.

"Mimi naishi kwa kibali cha Kazi na Makazi tangu zamani wakati naingia hapa, kwahiyo vigezo vya kupata Uraia ninavyo, nina kila sababu ya kuomba kwa kuwa Tanzania imenitambulisha kwenye Dunia, sikuwa na ustaa nchini kwangu lakini hapa nimepata jina na kupata michongo" amesema Christian Bella.

Aidha msanii huyo ameendelea kusema "Watanzania  walinikubali na kunipa nafasi mpaka leo hii nimetimiza ndoto zangu kadhaa ambazo nilikuwa nazo, siwezi kuweka wazi gharama ninazolipia kuishi hapa ila ni pesa nyingi sana na nalipia kila baada ya miaka miwili" ameongeza.

Christian Bella ni mmoja wa wasanii ambao watakuwepo kwenye ziara ya muziki ya AliKibaUnforgettable Tour, akiwemo na Tunda Man pamoja na kundi la Kings Music, siku ya Disemba 21, 2019, mkoani Iringa.