Thursday , 29th Aug , 2019

Afisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa kauli mbiu yao ya 'Kupapasa' tayari imeanza kujengeka kwa mashabiki wa soka baada ya kuwafunga Yanga hapo jana katika mchezo wa ligi.

Masau Bwire

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Masau Bwire amesema kuwa kwa sasa Ruvu Shooting haina utani tena na ikitoa ahadi ya kupapasa, ni lazima iitekeleze.

"Ruvu Shooting wakikuambia wanakuja kukupapasa basi ujue wanakupapasa kweli na nikasema alama hiyo inaanza kujengeka kwa Yanga. Tayari alama ipo kwenye vichwa vya Watanzania kwamba hawa jamaa wanapapasa kweli", amesema Masau Bwire.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara VPL hapo jana, Yanga ilikubali kichapo cha bao moja kutoka kwa Ruvu shooting na kuweka rekodi ya kupoteza kwa mara ya kwanza dhidi ya timu hiyo katika misimu mitatu ya karibuni.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amekaririwa akisema kuwa chanzo cha kupoteza mchezo huo ni kutokana na uchovu wa wachezaji wake kwakuwa hawakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika, huku akiitupia lawama Bodi ya Ligi kwa kukataa ombi lao la kusogeza mbele  mchezo huo.