Tuesday , 9th Sep , 2014

Wizara tatu za maliasili na Utalii, wizara za mambo ya ndani ya nchi na ile ya mifugo na uvuvi zimeanzisha kikosi kazi cha pamoja kwa ajili ya kukabiliana na ujangili, uwindaji haramu pamoja na uhalifu katika bahari ya Hindi.

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mh. Lazaro Nyalandu.

Kikosi hicho kitaanzishwa kwa msaada na ufadhili wa kamati ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira na maliasili ambayo inaoongozwa na nchi wahisani ya International Conservation Group, kamati inayotokana na mkutano pamoja na kampeni ya kimataifa iliyoongozwa na rais Jakaya Kikwete kuhusu vita dhidi ya ujangili.

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja baina ya serikali na nchi wahisani, waziri wa maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu na naibu waziri wa Mambo ya ndani Pereira Ame Silima wamesema uundwaji wa kikosi hicho utahusisha aina zote za uhalifu wa rasilimali za maliasili, uharamia pamoja na uhalifu unaotokea katika ukanda wa bahari.

Awali, Serikali ya China imeahidi kupambana na biashara ya magendo hususani ya bidhaa zinazovushwa na kuingizwa nchini humo zikitokea Tanzania.

Balozi Youqing ametaja baadhi ya biashara ambazo serikali yake itaendelea kuzipiga vita kuwa ni pamoja na ile ya meno ya tembo na bidhaa zinazotokana na wanyamapori ambao uwindaji wake umekatazwa kutokana na kuwa katika hatari ya kutoweka.

Wakati huo huo, Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema itaendelea kuweka mikakati ya kupambana na biashara haramu ya binadamu kwani Watanzania hawatakiwi kushiriki na kuigeuza biashara hiyo kuwa ndio chanzo chao kikuu cha kipato.

Msemaji mkuu wa idara ya uhamiaji Bw. Abbas Irovya, amesema hayo leo kufuatia kile alichodai kuwa ni kukithiri kwa biashara haramu ya binadamu inayofanya na mtandao wa uhalifu wa kimataifa unaovusha wahamiaji haramu kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Akifafanua kuhusu mtandao huo, Bw. Irovya amesema wahamiaji haramu kutoka nchi za Pembe za Afrika, wamekuwa wakisafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa kulipa pesa kwa wahusika wa mtandao huo ambao nao hugeuza kuwa ndio biashara na chanzo kikuu cha mapato.