Tuesday , 6th Aug , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wiki ya maonesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Agosti 6, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara ya kukagua mabanda kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri, nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amesema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazozalishwa nchini.

Tumetoa fursa kwa nchi za SADC zote nao pia waoneshe bidhaa zao. maonesho haya ni ya wazi, Watanzania wanayo nafasi ya kuja kuona na kujifunza,” amesema  Waziri Mkuu