Monday , 29th Jul , 2019

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Dodoma, inawashikilia baba na mwanaye kwa kosa la kuahidi na kutoa hongo ya shilingi milioni moja na laki mbili kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi.

Majina ya watuhumiwa hao ni Bahadur Abdalah Hirji (Baba) mfanyabiashara na mwanaye Nahid Bahadur Hirji ambaye ni Mhasibu, ambao inaelezwa walitoa kiasi hicho cha fedha ili kumfanya DC Katambi, asifuatilie mapungufu katika utekelezaji wa amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma  ya kukazia hukumu iliyowasilishwa kwake na dada wa Bahadur Hirji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 29 na Mkuu wa TAKUKURIU Mkoani humo Sosthenes Kibwengo,  imeeleza kuwa baada ya kupata taarifa hizo, walianza kufuatilia na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao Julai 27 majira ya saa kumi jioni,  katika Hotel ya Royal Village Area D mara baada ya mtuhumiwa Nahid kumkabidhi Mkuu wa wilaya rushwa hiyo.

Aidha TAKUKURU Mkoani humo inatarajia kuwafikisha mahakamani takribani watu saba, ambao wanashikiliwa kwa vitendo vya kujihusisha na kuomba na kupokea rushwa pamoja na  kuahidi na kutoa rushwa.