Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Atazungumzia pamoja na mambo mengine, mchakato wa Katiba mpya ambao umeibua mvutano mkubwa baada ya wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujiengua. Habari zinasema kuwa Rais Kikwete atakutana na viongozi hao leo saa 5 asubuhi.
Chanzo kimoja cha habari kutoka TCD ambacho hakikutaka kuandikwa jina lake, kililiambia NIPASHE jana kuwa, Rais Kikwete baada ya kumaliza kukutana na viongozi hao, atakutana na wajumbe wa TCD kwenye ukumbi wa St. Gasper mjini hapa.
“Naomba nieleweke kwamba TCD si Ukawa bali ni Kituo cha Demokrasia Tanzania ambacho kinajumuisha vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa,...lakini nashangaa waandishi mnavyosema Ukawa kukutana na Rais,” kilisema chanzo hicho.
Alisema wenyeviti na makatibu wakuu watakaokutana na Rais Kikwete ni kutoka vyama vya CCM, Chadema, UDP, TLP, NCCR Mageuzi, CUF na visivyo na wawakilishi bungeni.
Kikao hicho kinafanyika huku kukiwa na hisia tofauti kuhusiana na Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Baadhi ya wananchi na makundi ya kijamii yamekuwa yakiwataka wajumbe waliosusa (Ukawa) kurejea bungeni kuungana na wenzao waliobaki kutengeneza Katiba yenye maridhiano, huku wengine wakimtaka Rais Kikwete kulisitisha kwani Katiba itakayopatikana bila Ukawa itakuwa si ya maridhiano.
Kwa upande wao, Kundi la wajumbe wa Bunge Maalum la Katika kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi - UKAWA, lililosusia mchakato wa Katiba kupitia mfumo rasmi, limesema halina mpango wa kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa sasa kwani lilishakutana naye mwishoni mwa mwezi Juni, mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa umoja huo, Tundu Lissu, alisema hata yeye anasikia kwenye vyombo vya habari kuwa umoja huo unatarajiwa kukutana na Rais Kikwete.
“Mwenyekiti wetu, (Freeman Mbowe) alikutana na Rais Kikwete mwishoni mwa Juni na mwanzoni mwa Julai, kabla hatujaanza kukutana na Kinana (Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana) na kufanya mazungumzo na CCM yaliyodumu kwa takriban mwezi mzima,”alisema Lissu.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani, alisema wangetaka kuonana na Rais Kikwete wasingelazimika kuandika barua kuomba hilo bali wangepiga simu tu na kuzungumza, kupanga namna ya kukutana naye.
Awali, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu jana, Salva Rweyemamu, amekaririwa akisema kuwa amekanusha taarifa zilizoenea kwamba Rais Kikwete atakutana na Ukawa, na badala yake akasema atakaokutana nao ni viongozi wa vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
“Kwani Ukawa wameomba kukutana na Rais? Wanahabari tunatakiwa kujiridhisha kabla hatujapeleka taarifa kwa umma, ni vizuri kuuliza kila anayetajwa kwenye taarifa ambayo mtu anashughulikia ili kupata uhakika wa taarifa husika, ninachofahamu atakutana na TCD siyo Ukawa”, alisema.