Kocha na wachezaji wa Yanga
Akizungumza na www.eatv.tv, kocha Zahera amesema kuwa wachezaji hao hawakumpa taarifa yoyote juu ya mgomo wao na kuwataka kubadili msimamo.
"Wachezaji hawa nadhani maisha yao yote wako na mimi hapa, Ninawasidia mambo ya nje ya uwanja pia tangu nilipofika hapa. Nadhani wengi wao waliofanya hivyo leo, wangefikiria mara mbili badala ya kuwafuata tu ushahuri wa wake zao ambao wamewaambia wagome mazoezi", amesema Zahera.
"Wamefanya kitu hicho bila kunipasha. Nimetumwa na Hafidh niwaambie kuwa yeyote atakayekosa mazoezi ya kesho basi abaki nyumbani kwake mpaka mwisho wa ligi. Hawezi kucheza tena, na wanajua mwezi gani wa mwisho kupata mishahara yao, inakuwaje wanagoma leo mwezi mmoja kabla ya ligi kuisha?. Kwahiyo msimamo wangu ni kwamba atakayegoma kesho namuondoa".
Zahera pia amejibu kauli ya Afisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyemtuhumu kuwa amemsema vibaya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji kuwa aliwahujumu Yanga ili wafungwe katika mchezo wa ligi wa watani wa jadi.
Kocha Zahera amesema, "kuhusu suala la Manara na Cannavaro ni kwamba Manara anazungumza vitu vingi sana vya hovyo, sasa kama anasema ananishtaki kwa sababu ya Cannavaro kwanini haendi moja kwa moja kunishtaki?".
Yanga hivi sasa ipo jijini Dar es salaam wakijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 29 katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.