Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi nchini Tanzania, mhe. Mwigullu Nchemba.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi matawi hayo, Naibu Waziri Nchemba ameipongeza UTT MFI kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya muda mfupi kwa kuweza kuwa na matawi 10 na kusambaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Serikali imefurahi kuona kuwa mna dhamira na nia ya kweli ya kuhakikisha mnasambaza huduma zenu katika kila pembe ya nchi yetu. Hii inajionyesha, kwa kuwa tayari mmeshaanza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo aina 8 za mikopo, huduma za uwakala wa Bima, Uwakala wa Benki, uwakala mkuu wa mitandao ya simu (Mobile Money Super Agent) na yote haya ni ndani ya mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwenu”.
Waziri ameweka wazi kuwa serikali iliamua kwa makusudi kuanzisha taasisi hiyo ili kuwawezesha kiuchumi wananchi hususan wale wenye miradi/biashara ndogondogo na za kati ambao wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika kupata mikopo na huduma nyingine za kifedha toka taasisi kubwa za kifedha na mabenki ya biashara ambayo mara nyingi muundo na mfumo wa taasisi hizo huambatana na masharti magumu, hususani kwa wenye vipato vya chini, ikiwepo sharti la dhamana ya mali isiyo hamishika kama nyumba, kiwanja na mali nyingine.
Amesisitiza kuwa ni matumaini ya Serikali kuwa kuanzishwa kwa UTT Microfinance kutachochea ukuaji wa uchumi na kuwainua watanzania walio wengi. “Bila shaka huduma zenu zitaleta mapinduzi makubwa sana katika kumuinua Mtanzania wa kawaida kimapato na hatimaye kukuza ustawi wa jamii, na kuimarisha uchumi wa Taifa letu” alisisitiza waziri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UTT MFI Balozi Fadhili Mbaga, alisema watahakikisha kuwa UTT MFI inatekeleza azma yake kwa ufanisi na pia itashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali. “Tunapenda kusisitiza dhamira yetu ya kuendelea kushirikaiana na wadau mbalimbali hususan Tanzania Microfinance Association katika jitihada za jumla za kuwa na mfumo mzuri wa huduma za kifedha na mitaji midogo na kuhakikisha kuwa huduma hizi zinawafikia watanzania wengi zaidi na kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya jamii yetu”.
Balozi Mbaga aliongeza kuishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa inayotoa kwa taasisi hiyo. “Tunashuikuru sana kwa ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka serikalini. Hii ni changamoto kwetu kuhakikisha kuwa tunavuka malengo tuliyojiwekea na tunaiomba serekali isisite kutuunganisha na wabia na washirika mbalimbali ili tuweze kuwa na mtandao mpana zaidi na tuweze kuwa na nguvu kuwa ya kuwafikia wananchi wengi zaidi” alisema Balozi Mbaga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT MFI James Washima amesema wanaamini kuwa Serikali haikufanya makosa hata kidogo katika kuanzisha UTT MFI. “Kwa uzoefu wetu wa mwaka mmoja, tumegundua kuwa huduma za kifedha na mikopo hususan kwa wajasiriamali na watanzania wa kada za kati na chini ni kitu ambacho kilikuwa kinasubiriwa kwa hamu kubwa sana” alisema Washima na kuongeza “Kiu hiyo ya Watanzania kwa huduma zetu imedhihirika pale tulipokabiliwa na changamoto ya muitikio mkubwa wa watu kuliko matarajio yetu kiasi kwamba ndani ya miezi sita tu tulilazimika kuongeza idadi ya wafanyakazi kwani kwa wale waliokuwepo ilifika wakati mfanyakazi mmoja anahudumia wateja zaini ya 1,000. Huu ni muitikio mkubwa na mzuri kutoka kwa jamii na sisi tunajitahidi kukabiliana nao kwa ufanisi” alisisitiza.
Akibainisha mafanikio yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja wa uwepo wa sokoni, Washima alisema kuwa wameweza kukuza mtaji wa Taasisi toka Shilingi billion 5.4 mnamo Julai mwaka 2013 na kufikia bilioni 12 mnamo Juni, 2014.
Pia taasisi imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh 5.316 bilioni, kwa wakopaji 6,102 – huku 84% ya wakopaji wote wakiwa ni wanawake na kwamba tayari wameanzisha huduma mbalimbali ambazo zinamlenga moja kwa moja muhusika (Tailor-made) kama vile mikopo kwa ajili ya Bima ya matibabu, Hati Malipo (Contract Financing loans), mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo (Group loans), Mikopo kwa ajili ya SACCOS, Mikopo maalumu kwa miradi inayolenga kuongeza thamani ya bidhaa na ajira ikiwemo viwanda vidogo vidogo, mikopo kwa wafanyakazi wa Serikali, nk
Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, Washima alieleza baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuibuka kwa taasisi na kampuni zisizo rasmi ambazo hutoa huduma za kifedha hususan mikopo kwa watu wa kada za chini, lakini mengi ya makampuni haya mara nyingi huwa ya kilaghai na yenye kuchukua riba kubwa sana na bila utaratibu maalum suala ambalo badala ya kuwasaidia watu, huwaumiza na kuwaua kabisa kiuchumi.
“Tunaiomba serikali iharakishe utungwaji wa sera ya kurasimisha huduma hizi ili zifanywe kwa utaratibu maalum na pia ziratibiwe na kudhibitiwa vizuri ili wananchi wasiendelee kutaabika na kufilisiwa na watu wasio na nia njema ambao hutumia fursa ya udhaifu wa kisera kujinufaisha” alisema Washima.
UTT MFI ni Taasisi ya huduma za fedha na mikopo iliyoanzishwa mnamo Juni 2013 kwa lengo kuu la kutekeleza sera za serikali katika uwezeshaji kiuchumi hususan kwa wajarisiamali, watumishi wa umma, wakulima, wenye viwanda vidogo, watu wasio na ajira rasmi na wananchi wote kwa ujumla.
UTT MFI pia inalenga kuwapa fursa wamiliki wa Vipande vya UTT AMIS kutumia vipande vyao kama dhamana wakati wa kuchukua mikopo, kupanua wigo na kurahisisha uwekezaji wa vipande vya UTT na hivyo kukuza utamaduni wa kuwekeza kwa wananchi.