Thursday , 14th Aug , 2014

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi wamekutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili namna chama hicho kitakavyoweza kuleta umoja utakaofanikisha kupatikana kwa katiba mpya.

Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia.

Akizungumza na EATV muda mfupi baada ya kufungua kikao hicho Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mh. James Mbatia amesema kikao hicho pia kimetoa msimamo kwa wabunge wake 7 ambao kama watahudhuria kikao cha bunge maalum la Katiba watakuwa wamejifukuzisha wenyewe ndani ya chama hicho.

Kuhusu ushiriki wa chama hicho katika uchaguzi Mkuu ujao Mh. Mbatia amesema wajumbe hao watatoka na maazimio ambayo yanalenga kuhakikisha vyama vya siasa vinashiriki katika uchaguzi mkuu huo katika mazingira ya uwazi ambayo yatasaidia kuondosha udanganyifu utakaoweza kujitokeza.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Tanzania Dr Garib Bilal amewataka wadau wa elimu ya juu hapa nchini kujadili changamoto zinazokwamisha ukuwaji wa elimu ya juu ili kukuza elimu hiyo kwa viwango vya kimataifa katika kufikia malengo ya millennia ifikapo 2015

Dr Bilali ameyasema hayo katika ufunguzi wa kongamano la 6 la vyuo vikuu jijini Arusha, ambapo amesema kwa sasa malengo hayo kwa shule za msingi yamefanikiwa hiyvo kazi kubwa inabaki kwa wadau hao, kuhakikisha kongamano hilo linakuja na mikakati endelevu.

Aidha ameongeza kuwa ili kuwa na elimu endelevu ni lazima wadau waweke sera zinazoendana na sera za nchi na Jumuiya ya Afrika Mashariki ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika sekta ya elimu ya juu.