Sunday , 28th Oct , 2018

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amewataka wananchi kutokaa kimya yanapotokea matukio ya utekaji nchini, akibainisha kuwa kukemea kunasaidia ukweli kujulikana na hata wahusika kupatikana na kuongeza kuwa kelele za umma zimesaidia kupatikana kwa mfanyabiashara Mo Dewji.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

Zitto ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 28, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam, ambapo amesema Watanzania kupaza sauti baada ya kutekwa na kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ kumesaidia kupatikana haraka.

"Mshikamano ambao watanzania tulionyesha kwenye swala la Mohamed Dewji limeifundisha dola kwamba wananchi wamechoka na vitendo vya utekwaji na mauaji ya raia nchini", amesema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo ameongeza kuwa, “Haya tumekuwa tukiyasema ndani na nje ya Bunge na tutaendelea kusisitiza kwa sababu tunafahamu umuhimu wa vyombo hivi, na kama wapo wachache wanaochafua taswira ya vyombo hivi ni lazima tuseme".

Zitto Kabwe pia, ameliomba Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya kina kuhusu tukio la mapigano kati ya askari na wananchi jamii ya Wanyantuzu wilayani Uvinza mkoani Kigoma lililotokea takribani siku 10 zilizopita.