
Ammy Ninje kushoto na Giaani Infantino kulia.
Baada ya jana Oktoba 22, 2018 shirikisho la soka nchini TFF kumtangaza rasmi kocha Ammy Ninje kuwa mkurugenzi wake wa ufundi, pia limeainisha majukumu yake ambayo yanakwenda sambamba na malengo ya rais wa FIFA ya kuhakikisha mpira wa miguu unasambaa kote.
Kwa mujibu wa TFF majukumu maalum ya mkurugenzi ni kuongoza mpango wa maendeleo na dira ya shirikisho katika masuala ya ufundi pamoja na kuhakikisha anafanya tathmini ya ufundi katika ngazi mbalimbali za soka nchini ikiwemo ligi kuu na madaraja mengine.
Jukumu jingine ambalo ni sehemu ya mipango ya FIFA katika kuhakikisha soka linaendelea, ni mkurugenzi kuhakikisha elimu ya soka inatolewa kwa makocha kwa kuandaa na kusimamia kozi mbalimbali za ufundi.
Ili kwenda sambamba na mahitaji ya ufundi katika ligi, ni jukumu la Mkurugenzi kusimamia vilabu kuajiri makocha wenye sifa na taaluma inayoendana na daraja la timu anayofundisha, na hapa ndipo leseni za makocha zinahusika.
Kubwa zaidi katika yote ambacho ndio kimekuwa kilio cha Rais Infantino ni mkurugenzi kuhakikisha anaandaa mpango wa kukuza soka kwa wakati ujao kwa kuhakikisha soka la vijana linakuwa na kuendelea kwa manufaa ya baadaye.