Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha
Watuhumiwa 19 wanaohusishwa katika mtandao wa kulipua mabomu katika mikusanyiko na kuwamwagia tindikali viongozi wa dini wamepandishwa kizimbani leo katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha na kusomewa mashitaka mbalimbali yakiwemo ya mauaji.
Watuhumiwa hao ambao wameunganishwa na wenzao zaidi ya 20 waliokwishafikishwa kwenye mahakama hiyo kwa tuhuma hizo wamefikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao hajawahi kuonekana katika siku za hivi karibuni.
Tofauti na ilivyokuwa hapo awali ulinzi katika mahakama hiyo uliiimarishwa kwa kiasi kikubwa kuanzia mapema alfajiri ambapo watu wote waliokuwa wanaingia kwenye lango la mahakama hiyo walikaguliwa na vifaa maalumu, utaratibu ambao ulifuatwa na watu wote bila kujali nyadhifa zao wakiwemo watendaji wa mahakama hiyo.
Baada ya kufikishwa mahakamani hapo mbele ya hakim Devota Msofe aliyekuwa anasaidiwa na waendesha mashtaka Agustino Kombe, Felexs Kwetukia na Maselina Mwamunyange, washtakiwa hao walisomewa mashtaka yanayowakabili kwa makundi, jinsi wanavyodaiwa kuhusika na madhara yaliyosababishwa na makosa hayo.
Miongoni mwa mashitaka waliyosomewa ambayo kila mmoja alihusishwa kwa namna moja ama nyingine huku baadhi yao wakijikuta wakitajwa karibu kwenye makosa yote ni pamoja na shtaka la mauaji , kujihusisha na vitendo vya kigaidi , kukusanya silaha yakiwemo mabomu , kuyasafirisha na kisha kuyatumia kuua na pia kufadhili vitendo hivyo kwa kutoa fedha na ushirikiano wa kuvitelekeza.
Mashtaka mengine ni pamoja na kushawishi na kuhamasisha vijana kujiunga na vikundi vya ugaidi, kuhifadhi zana na silaha kwa lengo la kufanya ugaidi na kuzitumia kutekeleza vitendo hivyo.
Kesi ya watuhumiwa hao ambao wote wanahusishwa na matukio yote ya milipuko ya mabomu na kuwamwagia viongozi wa dini tindikali vilivyowahi kutokea mkoani Arusha itatajwa tena tarehe 15/08/2014 na washtakiwa wote wamerudishwa rumande ambapo kwa mujibu wa sheria kesi yao haina dhamana