
Kushooto ni aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Marehemu Mwl. Kasuku Bilago, Kulia ni Mgombea Elia Michael aliyeteuliwa na CHADEMA kugombea kiti kilichoachwa na Bilago.
Akizungumza na www.eatv.tv, Sosopi amesema kwamba CHADEMA imeendeelea kuwa kimbilio kwa vijana wenye ndoto ya uongozi ndiyo maana pasipokuangalia umri na uwezo wala mali wameweza kumpitisha kijana huyo kwenda kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mwl. Kasuku Bilago aliyefariki Mei 26 mwaka huu .
Sosopi amesema kuwa kashfa iliyowahi kutamkwa na aliyekuwa mtangulizi wake katika nafasi ya uongozi BAVICHA, haitakuwa na nafasi kwa kuwa Kijana Michael anaenda kushindana kwenye uchaguzi na watu waliowahi kushika uongozi huku yeye akiwa na umri wa kati wa miaka 25.
"Tunakishukuru chama kwa kutuamini vijana. Kimezidi kutupatia heshima na kutuamini. Tunaahidi hatutaweza kuwaangusha. Elia ni mdogo lakini tumejiandaa kwenda kutetea nafasi na heshima ya Bilago aliyoiacha Buyungu," Sosopi.
Akizungumzia kuhusu muungano wa ACT-Wazalendo na CHADEMA katika jimbo hilo, Sosopi amekishukuru chama hicho kwa kuweza kumpatia ushirikiano mgombea wao ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyowekwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wwa jimbo hilo, Mwl. Bilago.
"Viongozi wetu wanajua wapi tunatakiwa kwenda, tunaishukuru ACT kwa kutuunga mkono na kumpa ushirikiano mgombea wetu. Maneno ya kwamba maamuzi ya muungano yalifanywa na viongozi hatupaswi kuyapinga saizi kwa
kuwa tukio lililotokea lilikuwa la dharura na ndiyo maana kimetokea kitu kama hiki, lakini tunapaswa kuheshimu kwa kuwa wote tuna lengo moja la kuing'oa CCM na sasa si wakati wa upinzani kuanza kushindana," Sospi.
Hata hivyo mbali na CHADEMA kutangaza mgombea wao Kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoketi leo jijini Dar es Salaam kimemteua Ndg. Christopher Kajoro
Chiza kuwa Mgombea wa ubunge katika Jimbo la Buyungu kwa tiketi ya chama hicho.
Ndg. Chiza mwenye umri wa miaka 65 anakwenda kugombea nafasi hiyo ikiwa ni baada ya miaka miwili kupita tangu aliposhindwa kwenye uchaguzi mkuu 2015 na marehemu Kasuku Bilago.