Saturday , 19th Jul , 2014

Wakulima zaidi ya 1000 wanaojihusisha na kilimo cha zao la chai wilayani Lushoto na Korogwe wamemuomba waziri mkuu Mizengo Pinda kushughulikia mapema zoezi la kufunguliwa kwa kiwanda cha kusindika chai cha mponde kilichopo wilayani Lushoto.

Baadhi ya mashamba ya chai wilayani Korogwe mkoani Tanga

Wakulima zaidi ya 1000 wanaojihusisha na kilimo cha zao la chai
wilayani Lushoto na Korogwe wamemuomba waziri mkuu mheshimiwa Mizengo
Pinda kushughulikia mapema zoezi la kufunguliwa kwa kiwanda cha
kusindika chai cha mponde kilichopo wilayani Lushoto kufuatia asilimia
80% ya wakulima kuuza majani ya zao hilo kwa bei ya hasara kwa sababu
ya kukosa soko.

Wametoa kauli hiyo wilayani mufindi wakati wakizungumza na viongozi wa
taasisi ya taifa ya utafiti wa zao la chai nchini yenye makao makuu
yake wilayani humo, wakati wakulima hao walioongozwa na viongozi wa
serikali ngazi ya wilaya ya Korogwe walipotembelea kituo hicho kisha
kujengewa uwezo wa kujua mbinu na mikakati ya kuimarisha zao hilo
ambalo ndio tegemezi kwa uchumi wa wilaya za Korogwe na Lushoto mkoani
Tanga.

Baadhi ya wakulima ambao awali walikuwa wakiuza majani yao ya zao la
chai katika kiwanda cha mponde kilichofungwa mwaka mmoja uliopita kwa
sababu ya migogoro inayodaiwa kuhusishwa na sababu za kisiasa, wamesema
 awali walikuwa wakiuza chai kwa bei yenye maslahi lakini hivi sasa
wanauza katika kiwanda cha Ambangulu kwa bei isiyokuwa na tija
kufuatia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hatua ambayo baadhi yao
wamekata tamaa na kuyatelekeza mashamba yao.

Naye mkurugenzi mkuu wa kituo cha utafiti wa zao la chai nchini
Dr. Emmanuel Simbua akizungumza na wakulima hao katika kituo hicho
kilichopo Ngwazi wilayani Mufindi amesema kufungwa kwa kiwanda hicho
kumeathiri shughuli za kuhamasisha kilimo bora cha zao hilo kwa sababu
baadhi ya wakulima wamekata tamaa hivyo amewataka kuendelea na
jitihada za kuangalia zao hilo huku viongozi wakuu wa serikali
wakishughulikia tatizo hilo.

kwa upande wao wakuu wa wilaya za Mufindi na Korogwe wamewaomba
wakulima kuwa na subira na kwa sababu zao la chai katika wilaya hizo
ni tegemezi kwa uchumi wa kuanzia ngazi ya kaya na taifa hivyo lengo
lao ni kutaka kuwaongoza wananchi ambao wananufaika kiuchumi badala ya
kuilalamikia serikali katika sekta ya kilimo.