Sunday , 6th Jul , 2014

Meya wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam Yusuph Mwenda amewataka wananchi kutoa taarifa wanapoona dawa zenye nembo ya serikali zikiwa zinauzwa katika maduka binafsi.

Meya wa manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam nchini Tanzania Yusuph Mwenda amewataka wananchi kutoa taarifa mara moja pale wanapoona dawa zenye nembo ya serikali zikiwa zinauzwa katika maduka binafsi kwa lengo la kudhibiti wizi wa dawa za serikali na kuzwa kiholela katika maduka hayo.

Mwenda ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akifungua Zahanati ya Kata ya Manzese ambayo itaweza kuhudumia zaidi ya wakazi 10,000 wanaoishi katika Kata hiyo.

Meya Mwenda amesema kama wizi wa dawa za serikali hautadhibitiwa wananchi wataendelea kukosa dwa za matibabu katika vituo vya afya vya serikali hivyo ni wajibu wa wananchi kwa kushirikiana na serikali kufanya jitihada za kuwabaini watu hao.

Wakati huo huo, wakazi wanaoishi pembezoni mwa barabara ya Mabatini jijini Dar es salaam nchini Tanzania wameiomba serikali kuweka matuta katika barabara hiyo ili kuzuia ajali zinazotokea maramara kutokana na watumiaji wa vyombo vya moto kwenda kwa mwendo kasi .

Wakizungumza na East Africa Radio wakazi hao wamesema licha ya viongozi wa serikali kupita na kuona namna magari yanavyopita kwa kasi lakini hakuna jitihada zozote ambazo serikali inazichukua za kuhakikisha barabara hiyo inawekwa matuta.

Wakazi hao wamesema wamekuwa wakishuhudia ajali za mara kwa mara kutokana na mwendo kasi wa magari lakini iwapo serikali itaweka matuta barabara hiyo ajali hizo zinaweza kuzuilika.