Friday , 5th Jan , 2018

Mfanyabiashara James Rugemarila ambaye akabaliwa na kesi ya kutakatisha fedha na kuhumu uchumi, amewataja wahusika wakuu wa wizi wa fedha za serikali zilizoisababishia nchi hasara ya trilioni 37 kwenye sakata la Escrow.

Akizungumza katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, Rugemarila amesema ameshawasilisha nyaraka zake kwa TAKUKURU kuionesha serikali nani mwizi mkuu wa Escrow.

“Mwizi ni benki ya Standard Chartered LTD ya hapa Tanzania na iliyopo kule Hong Kong, na ndizo zilizoisababishia serikali hasara ya trilioni 37, na pia nimewasilisha nyaraka zingine kwa TAKUKURU zikionesha wengine walioshiriki kwenye wizi huo, naomba Mungu niwe hai ili niwe shahidi upande wa mashtaka”, alisikika Rugemarila akiiambia Mahakama.

Sambamba na hilo Rugemarila amesema wezi hao sio wameiibia serikali tu, bali hata yeye mwenyewe kwenye kampuni yake ya VIP ambayo inawadai trilioni 16.

Kabla ya maelezo hayo Rugemarila alimuomba Hakimu ampe ruhusa ya kwenda nchini India kufanyiwa uchunguzi wa tatizo la kansa ambayo analo kwa miaka 9 mpaka sasa, lakini ameona ugonjwa huo umeanza kumrudia ka nguvu na kuhofia uzima wake.

Kwa upande wa mshtakiwa mwengine ambaye ni mmiliki wa kampuni ya IPTL Harbinder Seth Sigh ameiomba mahakama imruhusu kufanyiwa matibabu kutokana na tatizo lake la kiafya, kwani pia anatamani kuwa shahidi upande wa mashtaka kwa kuwa naye ameshawasilisha nyaraka zake kusaidia upelelezi.

Kesi hiyo imehairishwa mpaka Januari 19, 2017 itakaposikilizwa tena, huku Hakimu akiamuru upande wa upelelezi kuharakisha kukamilisha upelelezi wake.