
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Pascal Barandagiye, mchango huo unatolewa kwa hiari na wala si kwa kushurutishwa na kwamba, mchango utatolewa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari 1, 2018.
Wachangiaji wamewekwa katika makundi matatu. Wananchi ambao si wafanyakazi wa serikali watatoa mchango wa Faranga za Burundi elfu mbili sawa na kwa kila mwaka kwa kila familia, Faraga za Burundi 1,000 kwa mwaka kwa wanafunzi walio na umri wa kupiga kura na mchango kwa watumishi wa umma utatolewa kulingana na mishahara yao.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani Pascal Barandagiye amesema, mtumishi wa umma ambaye hatachangia atatakiwa atoe maelezo kwa barua na kuwasilisha barua hiyo kwa viongozi husika.
Wadadisi wanasema hata kama serikali imetangaza kwamba mchango huo unatolewa na raia yeyote wa Burundi kwa hiari yake, kuna hatari watu ambao watakua hawajschangia katika uchaguzi huo watakosa baadhi ya huduma kutoka ofisi za serikali, na hali hiyo inaweza kuwa miongoni mwa njia za kukuza au kuendeleza utawala wa kiimla nchini humo.
Burundi inaendelea kukabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Ulaya na Marekani, ambao ni wafadhili wa kubwa wa taifa hilo dogo la Afrika ya Kati, kufuatia msimamo wa serikali wa kukataa mazungumzo na upinzani na kuendelea kuvunja haki za binadamu.