
Mwesigwa amesema anashukuru Halmashauri ya Kamati Kuu na chama chake cha CCM, kwa kumpa nafasi ya kugombea Uenyekiti wa UVCCM, kati ya vijana 113 waliochukua fomu lakini pia kupata uteuzi kati ya vijana saba waliopitishwa na Halmashauri Kuu kugombea nafasi hiyo.
"Nimempigia simu Mwenyekiti aliyeshinda kumpongeza kwa kupata ushindi lakini pia kumuahidi kwamba nitampa ushirikiano wangu kwenye majukumu yake mbalimbali, pamoja na pongezi hizo yapo matendo ambayo hayakuridhisha katika uchaguzi wetu ikiwemo vitendo vya rushwa vilivyojitokeza kwa baadhi ya wagombea", amesema Mwesigwa.
Mgombea huyo pia amesema vitendo vya rushwa katika chama chao sio jambo jema kwani linashusha heshima ya chama na linakipunguzia nguvu chama, lakini anamshukuru mheshimiwa Rais kwa kukemea vikali vitendo hivyo vya rushwa na kuvipongeza vyombo vya dola kwa kuwakamata wale wote walioonekana wakijihusisha.
Katika uchaguzi huo wa UVCCM, Kheri James aliibuka mshindi kwa kupata kura 319 wakati Tobias Mwesiga aliibuka mshindi wa pili kwa kupata kura 127, Simon Kipala alipata kura 67, Kamana Juma alipata kura 27, Juma Mwaipaja naye alipata kura19, na Seif Mtoro aliambulia kura 16, huku Mganwa Nzota akipata kura 1.