Jeshi Stars waliingia kwenye 'grand finale' ya leo wakiwa sio tu hawajapoteza mchezo, bali hawajapoteza hata seti moja.
Mashindano ya mpira wa wavu kuwania ubingwa wa mkoa wa Dar Es Salaam yamefikia tamati leo kwa mchezo mkali wa grand finale kati ya watani wa jadi Jeshi Stars na Magereza na Jeshi Stars kuibukaq washindi kwa seti tatu kwa bila.
Mchezo huu umekumbushia fainali ya ubingwa wa taifa ya mwaka jana mjini Dodoma ambapo baada ya mchezo kuahirishwa mpaka siku ya pili kutokana na giza, Magereza waligoma kucheza wakitaka mechi hiyo ihamishiwe Dar
Mashindano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa ndani wa taifa, yaliendeshwa kwa mtindo wa ligi na mwisho wa siku timu yenye alama nyingi iwe bingwa. Katika mchezo wa leo, Jeshi Stars waliingia wakiwa hawajapoteza hata seti moja huku Magereza ambao ndio mabingwa watetezi waliingia uwanja wakiwa wamepoteza seti mbili licha ya kwamba hawakupoteza mchezo.
Kwa ushindi huo, jeshi Stars wamefanikiwa kuwavua ubingwa Magereza.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa wavu mkoa wa Dar Es Salaam 'DAREVA' bwana Siraju Hassan Mwasha ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo, amesema mashindano ya mwaka huu yamekuwa na ufundi na ushindani mkubwa kwa sababu timu zilitaarifiwa mapema hivyo zilijiandaa vya kutosha.
Nahodha wa Jeshi Stars Nassoro Sharif amesema ushindi huu ulikuwa muhimu kwao kuthibitisha uwezo wao mbele ya wapinzani wao wa jadi magereza.
Naye mchezaji mkongwe wa Magereza Fredy Said Mshangama amesema hawakujiandaa vya kutosha kwani mashindano haya hayakuwemo kwenye kalenda, lakini walishiriki ili kuokoa mchezo.
Mchezo huu unakumbushia fainali ya ubingwa wa taifa ya mwaka jana mjini Dodoma ambapo baada ya mchezo kuahirishwa mpaka siku ya pili kutokana na giza, Magereza waligoma kucheza wakitaka mechi hiyo ihamishiwe Dar kwani wao walikuwa tayari wamekwisha kata tiketi za basi kurudi Dar.
Katika sakata lile, Jeshi Stars ambao nao walishakata tiketi kama Magereza, walirudisha tiketi hizo ili wacheze mechi hiyo ya kiporo lakini Magereza hawakuonekana uwanjani kwani walikuwa tayari washarudi Dar. Kwa maana hiyo mechi ya leo ilikuwa na maana zaidi ya moja.