Friday , 30th May , 2014

Wananchi wa Babati mkoani Manyara wamemuomba Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kuingilia kati mgogoro wa ardhi ambao umekuwa ukiwanyima haki yao kwa muda mrefu.

Baadhi ya wakazi wa Babati wakiwa wamezuia msafara wa Abdulrahman Kinana katibu mkuu wa CCM

Watu wa jamii za kifugaji katika halmashauri ya Babati vijijini  wamelazimika kuzuia kwa muda msafara wa katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana ili asikie kero yao ya kudhulumiwa ardhi yao na mwekezaji kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji vya Vilima vitatu, Mausaa na Nkaiti

Wakizungumzia kero hiyo wakazi hao wamesema viongozi wa serikali za vijiji hivyo wamegawa eneo bila kuwahusisha na sasa wanafukuzwa na nyumba zao kuchomwa moto bila kuoneshwa mahali mbadala huku wakazi wa kijiji cha Galapo nao wakilalamikia kuongezwa kwa mipaka ya hifadhi na kuingia katika eneo la kijiji.

Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana  ameonesha kuchukizwa  na ongezeko la migogoro ya ardhi na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na watendaji kutoshughulikia kwa wakati matatizo ya wananchi na kuahidi kulishughulikia suala ilo.