Thursday , 2nd Mar , 2017

Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA), Joyce Kiria ameiomba serikali kuondoa kodi kwa wafanyabiashara wa bidhaa za taulo zitumikazo wakati wa  hedhi (Pedi) ili watoto wa kike waliopo shuleni waweze kuzimudu kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi HAWA Foundation, Joyce kiria

Kiria amesema serikali ina wajibu wa kuwasaidia mabinti wa shule wanaoishi katika mazingira magumu kwa kutoa misamaha ya kodi ili kuwanusuru wanafunzi wanaoshindwa kwenda shule ndani ya siku tano kwa kila mwezi wanapoingia kwenye mzunguko wa hedhi ambapo kwa mwaka si chini ya siku 60 hadi 70.

Hali halisi inaonesha kuwa wengi wa wanafunzi wa kike wamekuwa wakihatarisha afya zao kwa kutumia matambara kwa ajili ya kujisitiri wakati wa hedhi, hali ambayo pia imekuwa ikiwasababishia aibu pale vitambaa hivyo vinapovujisha damu ya hedhi na kubainika na wanafunzi wenzake shuleni.

ili kuondoa tatizo hilo, taasisi ya HAWA kwa kushirikiana na East Africa Television Limited, wanaendesha kampeni inayokwenda kwa jina la NAMTHAMINI, ikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwanunulia wanafunzi wa kike pedi hizo.

 

"Hakuna mwanamke ambaye anayeipenda hali ile ila tumezaliwa nazo, mimi na taasisi yangu pamoja na East Africa tumeona tusipige kelele nyingi pasipo kuonesha juhudi zetu kwenye vile vitu tulivyojaaliwa , hivyo tunaomba serikali na jamii kwa ujumla iungane na sisi ili kati ya wanafunzi 1,500 kila mmoja apate pedi za mwaka mzima".Joyce Kiria.

Ameongeza kwamba lengo la kampeni hiyo ni kumsaidia mwanafunzi kuwa salama anapokuwa katika siku zake za hedhi, hivyo wanakaribisha michango ya fedha na hata pedi zenye ubora mzuri uliothibitishwa kwa kupitia M-Pesa namba 5530307 au kupitioa akaunti ya CRDB namba 0150258750600.