Thursday , 2nd Mar , 2017

Msemaji wa klabu ya Ruvu Shooting Massau Bwire, amejikuta akifuta kauli yake iliyokuwa ikionesha tambo dhidi ya Yanga kuelekea mchezo wa jana kuwa timu yake ilishuka dimbani kwa ajili ya kuizika Yanga kwa madai kuwa tayari ilishauliwa na Simba.

Massau amesema licha ya kujipanga kwa ajili ya maziko hayo kwa kufuata taratibu zote za maziko, lakini walipokwenda 'mochwari' kuchukua mwili wa marehemu, wakashangaa kuona mwili huo ukipiga chafya hivyo kushindwa kuzika kama walivyokuwa wameahidi.

Ametumia mfano huo wa maiti kupiga chafya akielezea kipigo walichokutana nacho katika dimba la Taifa cha mabao 2-0 kutoka kwa mabingwa wa Tanzania, Yanga, huku akipeleka lawama zake kwa mwamuzi, kuwa ndiye aliyechangia kipigo hicho.

"Unajua wakati mwingine unaweza kujipanga kuzika lakini ukakutana na mambo ya ajabu, kilichotokea kwetu, ni maiti kugoma kuzikwa, tumefanya kila kitu, na kaburi limeshachimbwa, tumeandaa vifaa vyote vya kuzikia, lakini kwenda 'mochwari' kuchukua maiti, maiti ikapiga chafya, na yote hayo yamesababishwa na mwamuzi Simba kutoka Kagera, yeye ndiye aliyeharibu kila kitu, na hafai kuchezesha ligi kuu" Amesema Massau

Amesema klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kuiandikia barua TFF kumshitaki mwamuzi huyo kwa kuharibu mchezo huo wa jana, huku akilisifia bao lililofungwa na Obrey Chirwa wa Yanga kuwa lilikuwa ni bao halali, safi na zuri lakini mwamuzi alilikataa ili ku'balance' mchezo kwa kuwa alijua kuwa ametoa penati isiyo halali kwa Yanga

"Mzimu uliomtes mwamuzi hadi kukataa bao la Chirwa ni ile panati, alitoa penati ambayo haikuwa halali, sasa ili asionekane ametumwa kutuonea, akaanza kutafuta jinsi ya kubalance, mzimu huo ukamtesa akajikuta anakataa bao halali kabisa la Chirwa. Sisi tutaiandikia barua TFF kuepeleka malalamiko yetu" Amemalizia Massau