Rais Kikwete wa Tanzania (Kushoto) akifanya mazungumzo na Rais kabila wa DRC (Kulia)
Rais Jakaya Kikwete amewasili mjini Kinshasa , Jamhuri ya Watu wa Kongo (DRC)tarehe 9 Mei,2014 kwa ziara ya kikazi akitokea nchini Nigeria ambapo amehudhuria Mkutano wa Viongozi kuhusu Uchumi barani Afrika.
Akiwa Kinshasa, tarehe 10 Mei, Rais Kikwete atafanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila ambapo wanatarajia kuzungumzia uhusiano baina ya nchi mbili hizi na hali ya kisiasa kwa ujumla katika ukanda wa Jumuiya ya ushirikiano wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mara baada ya Mazungumzo haya Rais Kikwete anatarajia kuelekea Luanda , Angola kwa ajili ya mazungumzo na Rais Jose Dos -Santos
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Joyce Banda wa Malawi kufuatia kifo cha ghafla cha Balozi wa Malawi nchini Tanzania Flossy Gomile-Chidyaonga kilichotokea tarehe 9 Mei jijini Dar-Es-Salaam.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Balozi Chidyaonga, ni huzuni kwetu sote" Rais amesema na kumuelezea Balozi Chidyaonga kuwa alikuwa mcheshi na aliyependa kushirikiana na wenzake kwa moyo mkunjufu.
" Ni huzuni zaidi kwetu sote kwakuwa kifo chake kimetokea ghafla mno kwa mtu tuliekua tunashirikiana naye kwa karibu katika juhudi za kukuza na kuimarisha mahusiano baina yetu" Rais amesema na kuongeza kuwa , kifo chake kimetokea wakati tunamhitaji zaidi na hivyo kusababisha pengo kubwa"
Rais amemuomba Rais Banda kufikisha salamu zake binafsi na za Watanzania kwa ujumla kwa familia ya marehemu, ndugu, Jamaa na Wamalawi wote kwa ujumla na kumuombea marehemu kwa mwenyezi Mungu, ampe mapumziko mema milele.