Friday , 9th Sep , 2016

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imesema kuwa itawarudishia fedha zao, watu ambao watathibika kukatwa pesa licha ya kuwa hawakukopeshwa na bodi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa HESLB Abdul-Razaq Badru (Kushoto)

Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amekiri kuwepo kwa majina ya watu ambao walikuwa hawadaiwi na bodi hiyo, yaliyowekwa hadhani pamoja na orodha ya majina ya wadaiwa.

Badru amesema sababu kubwa ya kutokea kwa dosari hiyo ni waajiri kufanya makosa ama ya makusudi ama ya kutokujua, kwa kutuma majina ya waajiriwa ambao hawakukopeshwa na bodi hiyo

“Tulichokifanya tuliwaomba waajiri wote watutumie majina ya watu waliokopeshwa na bodi, lakini wakakosea, wakajumuisha na majina ya watu ambao hawakukopeshwa, kwahiyo kosa limefanyika kwa waajiri, kwahiyo kama kuna mtu hakukopeshwa lakini ameanza kukatwa, afike ofisini kwetu na taratibu za kurudishiwa pesa zake zitafanyika” Amesema Badru.

Ameongeza pia kuwa kila siku katika makao makuu ya bodi hiyo, watu humiminika wakiwa na malalamiko ya aina hiyo.

Hata hivyo Badru amesema kuwa mwitikio wa urejeshwaji wa fedha hizo ni mkubwa ambapo hadi sasa kati ya shilingi bilioni 300 wanazotarajia, tayari shilingi bilioni 105 zimekwisha rejeshwa sawa na asilimia 40.

Amesema pia kasi ya urejeshwaji wa fedha hizo kwa mwezi imeongezeka, kutoka shilingi bilioni 2 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 6 kwa mwezi na lengo ni kufikisha kiwango cha shilingi bilioni 8 kwa mwezi.

Aidha, amesema hadi sasa jumla shilingi trilioni 2.6 zimekwisha kopeshwa.