Mwanadada Serena Willams akishangilia baada ya kushinda fainali ya Wimbledon.
Gwiji wa tenisi upande wa kinadada Serena Williams ameshinda fainali ya michuano ya ubingwa wa michuano mikubwa ya tenisi Grand Slam ya Wimbledon na kuifikia rekodi ya mchezaji Steffi Grafs ya kutwaa Grand Slam 22 kufuatia hii leo kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Wimbledon baada ya kumduwaza Mjerumani Angelique Kelber kwa seti mbili mfululizo za michezo 7-5 na 6-3.
Serena mwenye umri wa miaka [34] ndiye aliyekua bingwa mtetezi wa michuano hiyo na sasa anaweka kibindoni taji la saba [7] la michuano hiyo mikubwa ya tenisi Wimbledon kwa kalenda ya michezo ya tenisi dunia.
Ushindi huo kwa Serena ni kama kulipiza kisasi dhidi ya Kelber kufuatia Mjerumani huyo kumshinda katika fainali ya michuano ya wazi ya Australia Iliyofanyika mapema mwaka huu mjini Melborne nchini Austalia.
Lakini pamoja na Serena Williams kufikia rekodi ya Gwiji wa Ujerumani Graf ya kuwa bingwa wa wakati wote wa michuano ya ubingwa mkubwa ama michuano mikubwa ya tenisi ya Grand Slam kwa mtu mmoja mmoja [singles], bado mchezaji huyo anakuwa nyuma mara mbili kwa mchezaji kiongozi wa muda wote wakutwaa mataji makubwa Margaret Court, ambapo raia huyo wa Australia yeye alishinda mataji 13 kati ya 24 katika michuano hiyo mikubwa wakati huo ikiwa ya ridhaa kabla ya baadaye kubadilika na kuwa ya kulipwa mnamo mwaka 1968.
Fainali nyingine ya mtu mmoja mmoja kwa upande wa wanaume itamkutanisha mwenyeji wa michuano hiyo Mwingereza Andy Murray ambaye ni mchezaji bora namba moja kwa sasa nchini Uingereza kwa upande wa wanaume akicheza fainali ya tatu ya michuano hiyo ambapo yeye atakuwa katika kibarua dhidi ya mchezaji Milos Raonic siku ya jumapili Julai 10 mwaka huu.