Wabunge hao wameziba midomo kwa kutumia karatasi na plasta na kutoka nje huku wabunge wa chama tawala wakiendelea na kazi yao kama kawaida na maswali ambayo walilenga kuuliza wabunge wa upinzani yakiulizwa na wabunge wa chama tawala kwa niaba yao.
Nje ya ukumbi wa Bunge wabunge hao wamesema wamefanya hivyo kuonyesha kwamba Bunge limekataa kusikiliza hoja zao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mbunge wa Jimbo la Vunjo James Mbatia amesema kwamba hawatakubali nchi hii iongozwe kwa fikra za mtu mmoja pia wanasikitishwa na kitendo cha wabunge wa chama tawala kuwatukana huku Naibu Spika akikaa kimnya.
''Hii ni ishara ya kuonyesha kwamba hasira zetu hatutakubali wakituzima midomo bungeni nje hawatatuzima juzi tumesusia hadi futari kuonesha kwamba hatukubaliani nao'' amesema Mbatia.
Aidha kwa muda wa wiki tatu mfulilizo wabunge wa upinzani wameendelea kususia Bunge kwa madai ya kuongozwa na Naibu Spika Tulia Ackson ambaye hawakubaliani na namna anavyoongoza vikao hivyo.