Wachezaji wa Twiga Stars wakiwa katika mazoezi.
Rais wa Jamhuri ya watu wa Rwanda Paul Kagame ameialika timu ya soka ya taifa ya wanawake ya Tanzania Twiga Stars kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mchezo maalumu wa kirafiki dhidi ya timu ya wanawake ya Rwanda utakaopigwa katikati ya mwezi Julai mwaka huu nchini humo.
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limethibitisha kupokea mwaliko huo wa Twiga Stars kupitia shirikisho la soka nchini Rwanda FERWAFA likiwataarifu juu ya mwaliko huo wa Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema tayari wameanza utaratibu wa kuwaweka kambini kwa siku chache mapema mwezi ujao nyota wa kikosi hicho kwa ajili ya kucheza mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki ambao umepewa umaalumu na Rais Kagame.
Aidha Alfred amesema mchezo huo maalumu umeandaliwa kwa mambo makuu matatu ambayo ndiyo lengo la kuchezwa kwake.
Lucas amesema moja la kwanza ni kutoa burudani kwa wakuu wa nchi ambao watakuwepo nchini Rwanda kwa ajili ya mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika AU utakaofanyika Julai mwaka huu.
Pamoja na kutoa burudani lakini kubwa ni kudumisha udugu baina ya nchi za Afrika hasa wao Rwanda na Tanzania na kupitia michezo itakuwa ni fursa kwao kufikisha ujumbe wa ushirikiano kwa haraka zaidi.
Sababu nyingine kubwa kwa rais Kagame ni pamoja na kuhamasisha wanawake kote barani Afrika kushiriki michezo kama soka hasa nchini kwake Rwanda kujaribu kuinua mwamko kwa kinamama [wanawake] kucheza michezo kwani sasa michezo ni ajira.
Kwa Wanyarwanda kwao itakuwa pia ni kipimo kizuri katika kujiweka sawa na michuano ya kimataifa hasa ikizingatiwa kwa siku za hivi karibuni tiu ya Twiga Stars imekuwa moja ya timu bora zinazotajwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, maziwa makuu na Afrika kwa ujumla hivyo kwao pia itakuwa ni kipimo kizuri sana kujua ubora wa kikosi chao.
Akimalizaia Lucas amesema kwa sasa wameanza kuwapa taarifa nyota wa Twiga Stars ili kuanza kujifua huko waliko kabla ya kuingia kambini kwa siku chache kwaajili ya mchezo huo na safari ya Rwanda mapema katikati ya mwezi ujao.