Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Haule akiwa pamoja na wachezaji na viongozi wa timu ya Taifa Stars.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dk. John Haule amewataka wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ambao wako nchini Kenya kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya wenyeji Harambee Stars kuhakikisha wanajituma na kuibuka na ushindi mnono katika mchezo huo na ule dhidi ya Misri kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika AFCON 2017.
Wito huo ameutoa barozi wakati alipokitembelea kikosi cha timu hiyo katika mazoezi yake ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho utakapoigwa katika dimba la Moi Kasarani jijini Nairobi ambapo pia balozi alikwenda kwa ajili ya kuwahakikishia usalama timu hiyo licha ya kuwako kwa taarifa za kuvamiwa.
Aidha, Balozi amewataka Taifa Stars kama kuna aina ya msaada wowote wanataka na chochote wanachohitaji amewaomba wamtaarifu ili wajue namna ya kuwasaidia mapema.
'Msiwe na wasiwasi kabisa, hata kama hamjaipenda hoteli mliofikia semeni,” aliwaeleza balozi huyo Dk. Haule ambaye mwisho akaitakia timu mafanikio mazuri katika mchezo wa dhidi ya Harambee na lakini kubwa ni ule wa Mafarao wa Misri kuwania kufuzu AFCON.
Viongozi wa msafara wa Taifa Stars, Ahmed Mgoyi na Omar Walii wamemweleza Balozi DK. Haule kuridhika na kambi na kwamba hawakupata tatizo lolote hali ilivyo hadi sasa na kimsingi wako tayari kwa mchezo huo wa kesho dhidi ya Harambee Stars.