Kikosi cha Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga ambacho kimeshashuka daraja kwenda daraja la kwanza FDL.
Pazia la msimu wa Ligi Kuu 2015/16 linatarajiwa kufungwa Jumapili ijayo Mei 22, mwaka huu na timu tano zinazoonekana kuwa katika hatari ya kuungana na Coastal Union yenye pointi 22 (nafasi ya 16) kushuka daraja. Kati ya timu hizo tano, mbili ndizo zitaungana na Coastal kushuka daraja hivyo kuwa na jumla ya timu tatu.
Timu zote za Ligi Kuu tayari zimecheza mechi 29 na ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15); Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao wakishinda.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Toto Africans itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Stand United, wakati JKT Ruvu mgeni wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wenyewe Kagera Sugar watamaliza na Mwadui FC watakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga wakati Mgambo wataalikwa Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ilihali African Sports ‘Wanakimanumanu’ wataifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi nyingine ya kukunja jamvi kwenye Ligi Kuu ya soka Tanzania bara zitakuwa kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Yanga itakayokuwa mgeni wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine wenye presha utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48 ambayo licha ya kucheza na Coastal Union ambayo imeshuka daraja kwenye Uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi ya nne. Mtibwa Sugar ina pointi 47.
Hakuna ubishi kwamba Tanzania Prisons itajizatiti licha ya kucheza na timu ambayo haina nafasi katika Ligi Kuu msimu huu. Presha kubwa ni kwa Simba na Azam ambazo zina tofauti ya pointi moja katika msimamo wa ligi hiyo iliyoshirikisha timu 16.
Azam FC ina pointi 63 ikishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga huku Simba inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 62. Mvutano wa Tanzania Prisons, Mtibwa ni wa nafasi ya tatu na nne hasa ukirejea kwenye zawadi za Vodacom ka timu vinara kama ilivyo kwa Azam na Simba.
Yanga ambayo imetwaa ubingwa, tayari imepewa taji na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji Jumamosi iliyopita na inachusubiri ni fedha Sh 81,345,723 wakati Azam na Simba zinawania zawadi ya mshindi wa Pili Sh 40,672,861 na Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 huku Prisons na Mtibwa Sugar zikichuana kupata zawadi ya Mshindi wa Nne ambayo ni Sh 23,241,635.
Pia timu zote zinawania zawadi ya Mchezaji Bora ambayo ni Sh 5,742,940 kiwango kinachofanana na atakachopewa Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa Bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom wakati Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 kiwango kinachofanana atakachopewa Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.