Sunday , 8th May , 2016

Mafanikio wanayopata makocha wazawa katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na hata katika timu ya taifa yamepelekea kocha mkuu wa timu ya soka ya Mwadui, Jamhuri Kihwelo kutamka sasa ni nafasi yao makocha wazawa katika ligi hiyo na timu za taifa.

Kocha Jamhuri Kihwelo wa Mwadui FC ya Shinyanga.

Kocha huyo mwenye maneno mengi ndani na nje ya uwanja Jamhuri Kihwelo akijulikana zaidi kwa majina ya kimichezo kama Julio Alberto Tarantin Chambamtu a.k.a Mourinho wa Tanzania amesema ni wakati sasa kwa vilabu vikubwa vya Tanzania kuwaamini makocha wazawa kwa kuwa wako wengi wenye uwezo mkubwa wa kufundisha kuliko hao wanaowang'ang'ania kwa sasa.

Julio amesema amengalia Ligi Kuu msimu huu na kugundua makocha wazawa wanauwezo kuliko wa kigeni ambao mambo mengi yanarahisishwa kwanza kwa uwezo wa kifedha wa timu husika na pia timu hizo kuundwa na wachezaji nyota waliosajiliwa kutoka vilabu vya ndani na nje ya nchi kitu ambacho kinawapa urahisi makocha wa kigeni kupata matokeo na kuonekana wao ni bora zaidi kuliko wazawa.

Aidha, Julio ambaye amewahi kuwa mwalimu wa timu za Kajumulo, Simba na Coastal Union ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Mwadui FC ya Shinyanga amesema kama wazawa watawezeshwa kama ilivyo kwa wageni basi matokeo ya timu zao yatakuwa makubwa zaidi ya haya kwa kuwa wao wanauzoefu wakukabiliana na changamoto na ugumu kuliko makocha wageni ambao mara nyingi viongozi wa vilabu vyao huwa wanawarahisishia kazi nje ya uwanja na kuwafanya makocha hao kuonekana wanauwezo na kuwalipa fedha nyingi.

Akimalizia Julio amesema ubora wao umeonekana katika michezo ambayo timu kama Mwadui anayofundisha yeye, Coastal Union ya Mzawa Idd Jangalu na hata Toto Africans ya John Tegete kuzisumbua sana timu kubwa kama Yanga iliyochini ya kocha Mholanzi Hans Van der Pluijm, Azam ya Mwingereza Stuat Hall, Simba ya Mganda Jackson Mayanja na Stand United ya Mfaransa Patrick Liewing.

Julio amekamilisha kwa kusema kutokana na mifano hiyo michache tu ni wazi huitaji mahesabu kupata jibu kuwa sasa ni vema makocha wazawa wakaaminiwa na kupewa nafasi katika vilabu vikubwa hapa nchini na hata timu za taifa akitolewa mfano mwingine kwa kocha wa taifa stars mzawa Charles Boniface Mkwasa 'Master' ambaye ameanza kwa mafanikio makubwa katika timu hiyo na siri pekee akibainisha ni kuaminiwa na kupewa nafasi sambamba na kuwezeshwa kwa kila kitu kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Mholanzi Mart Nooij.

Julio pia amefunga kazi kwa kusema katika kumbukumbu ya mafanikio ya timu za Tanzania katika michuano ya taifa na vilabu hakuna timu iliyofanikiwa ikiwa na kocha wa kigeni mfano mnamo msimu wa mwaka 1993/1994 Simba ilifika fainali za Kombe la Shirikisho Barani Afrika wakati huo ikijulikana kama michuano ya kombe la CAF ikiwa na kocha mzawa Abdalah 'King' Kibadeni 'Mputa' na hata timu ya Taifa Stars nayo ilikata tiketi ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1980 fainali zake zikipigwa Lagos Nigeria ikiwa chini ya makocha wazawa Joel Nkaya Bendera na marehemu Paul West Gwivaha.