Tuesday , 29th Mar , 2016

Vyama vya msingi Mkoani Mtwara (AMCOS) vimetakiwa kuweka wazi kwa kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi kwa wakulima wa korosho baada ya kufanyika kwa minada ili kuondoa malalamiko kwa wakulima ambao hawaridhishwi na wanachokipata.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, amesema bado hajaridhishwa na utendaji kazi kwa baadhi ya vyama hivyo na kuahidi kuchukua hatua kwa vyama ambavyo vitashindwa kutekeleza agizo hilo kuanzia msimu ujao wa korosho.

Amesema, amewaagiza maafisa ugani, wakurugenzi na wakuu wa wilaya wote kupita katika kila chama cha msingi kwa ajili ya kukagua taarifa na kujua kama wakulima wameridhia na walichokipata na kama bado zifanyike jitihada za dhiada kuweza kuwaridhisha.

Aidha, amesema katika msimu huu uliomalizika, mkoa umeweza kufika na kuvuka lengo kwasababu umeweza kukusanya jumla ya tani 100,006 huku lengo ambalo ulijiwekea ilikuwa ni kukusanya tani 90,000.