Monday , 21st Mar , 2016

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salum Jecha amewapongeza waangalizi wa uchaguzi wa marudio Zanzibar kwa kujitokeza kwao na kuona jinsi ambavyo zoezi hilo limeendeshwa salama.

Jecha ameyasema hayo alipokuwa akitangaza matokeo ya kiti cha Urais ambapo Mgombea Urais kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dkt Ali Mohamed Shein ametangazwa mshindi kwa asilimia 91.4% ya kura zilizopigwa.

Kwa mujibu wa bwana Jecha jumla ya waangalizi 1416 wameshiriki katika kuangalia mwenendo wa uchaguzi huo ambao huo kwa lengo la kuangalia mwitikio wa wananchi pamoja na namna zoezi zima lilivyoendeshwa.

Aidha Jecha amesema kwamba wagombea wote wa Urais14 walishiriki kwa sababu waliotangaza kujitoa walichelewa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ambapo walitakiwa kujitoa terehe 06 September 2016 siku walipoteuliwa.

Baada ya kukabidhiwa hati ya kumtambulisha kama Rais Mteule wa Zanzibar, mshindi Dkt. Ali Mohamed Shein amewashukuru wananchi kwa mwitikio wao na namna walivyo muamini kuwatumikia kwa kipindi cha pili.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna alivyoonyesha ushirikiani hasa katika kuimarisha ulinzi na usalama visiwani humo.