Wednesday , 16th Mar , 2016

Pamoja na kipigo cha bao 1-0 toka kwa vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara timu ya Simba, timu ya maafande wa ya Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya imesema bado ik katika mbio za ubingwa na hawajakata tamaa na watakomaa mwanzo mpaka mwisho.

Kikosi cha maafande wa magereza timu ya Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.

Tofauti na wengi wanavyodhani kuwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu unawaniwa na timu tatu pekee; Simba, Yanga na Azam lakini timu ya Tanzania Prisons maarufu kama "Wajelajela", nayo iko makini katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zao zilizobaki ili wachukue taji hilo.

Nahodha wa Prisons, Laurian Mpalile, ameeleza wazi mapambano yao, akibainisha kuwa nafasi bado wanayo na wamedhamiria kuhakikisha hilo linatimia, hivyo wanaendelea kupambana katika michezo yao iliyobaki wakianzia na mchezo wao wa jumapili ya wiki hii dhidi ya wenyeji wanakimanumanu Afrikan Sports kutoka jijini Tanga katika uwanja wa Mkwakwani.

Nanukuu “Nafasi bado tunayo, hatupo sehemu mbaya, naweza kusema hatujakata tamaa ya ubingwa na tunapambana katika hilo, nia yetu sasa ni kushinda katika michezo iliyobaki na kupata matokeo mazuri zaidi, ndiyo maana hata kwenye mechi yetu na Simba tulijitahidi katika hilo lakini tukapoteza mchezo dakika za mwisho,” alisema Mpalile.

Aidha Mpalile amesema kwa sasa suala la nani atakuwa bingwa ama timu gani zitashuka bado linabaki kitendalwili kwakuwa kila timu inauwezo wa kufanya jambo lolote katika michezo iliyosalia na kujiondoa katika nafasi iliyopo sasa na kupanda juu hiyo nafasi ya ubingwa bado iko wazi hasa kwa timu tano zilizo katika nafasi za juu wao wakiwemo.

Prisons kwa sasa inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 36 baada ya mechi zake 23, ikiwa imepishana kwa jumla ya pointi 18 na vinara Simba waliocheza mechi 23 na kukusanya pointi 54. Prisons imebakisha michezo saba, kama itashinda yote itakusanya pointi 21 jumla, lakini itaiombea Simba ipoteze mechi zake zote zilizobaki.