Baadhi ya madereva na abiria wakiwa wamesimama mbele ya mabasi katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo Mei mwaka jana.
Mgogoro huo kwa mujibu wa madereva hao utatokana na kusimama kwa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo, iwapo wataamua kugoma kufuatia kile walichokiita kuwa ni kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kushughulikia matatizo yao.
Wakizungumza kupitia kiongozi wao, Katibu wa Chama cha Madereva Bw. Abdallah Lubala, madereva hao wamesema wamechoshwa na kasi ndogo katika kushughulikia matatizo yao ikiwemo kutokuwepo kwa mikataba ya ajira, malipo na maslahi duni pamoja na unyanyasaji kutoka kwa waajiri wao ambao ni wamiliki wa vyombo vya usafiri.
Wamesema kuwa tangu kuundwa kwa kamati maalum ya waziri mkuu baada ya mgomo wa Mei mwaka jana, hakuna hatua yoyote iliyofikiwa zaidi ya kuendelea kuibuka kwa matukio ya unyanyasaji na vitisho kutoka kwa wamiliki, mojawapo baadhi yake yakiwa ni mauaji ya kutatanisha ambayo madereva hao wameyahusisha moja kwa moja na harakati za kudai haki zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Shaaban Mdemu, ameyataja mambo yanayoweza kuwalazimu kuingia katika mgomo kuwa ni kutokamatwa kwa mmiliki wa kampuni moja ya usafirishaji, anayetuhumiwa kumuua dereva wake kwa kumpiga risasi pamoja na lile la kuuawa kwa aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mdereva marehemu Rashid Saleh, ambaye inadaiwa kuwa kifo chake kimetokana na kulishwa chakula chenye sumu.