Friday , 26th Feb , 2016

Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau, Jose' Mario Vaz amemhakikishia Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali, hususani katika uchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau mara baada ya kupokea barua yenye Salamu na pongezi.

Rais Jose' Mario Vaz amesema hayo katika ujumbe wa barua uliwasilishwa kwa Rais Magufuli na Mjumbe maalum wa Rais huyo Jenerali Omar Embalo, Ikulu Jijini Dar es salaam.

"Napenda kusisitiza kuwa nchi zetu ni marafiki wa muda mrefu, naomba urafiki na mahusiano haya mazuri yaendelee na ninakuhakikishia kuwa nchi yangu itaendelea kuuenzi ushirikiano huu" Ilieleza sehemu ya ujumbe huo.

Aidha, Rais Jose Mario Vaz amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania katika awamu ya tano na amemualika kuitembelea nchi ya Guinea Bissau ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais Jose Mario Vaz kwa kumtuma mjumbe maalum kwa ajili ya kumletea ujumbe wa pongezi, na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Guinea Bissau.

"Nakushukuru sana Jenerali Umaro Sissoco Embalo kwa kuniletea ujumbe wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau na nakuomba umwambie namshukuru kwa pongezi, mimi na serikali yangu tupo tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Guinea Bissau ili mataifa yetu yaweze kunufaika zaidi" Alisema Rais Magufuli

Wakati huo huo, Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Ikulu Jijini Dar es salaam jana.