Wednesday , 9th Apr , 2014

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samwel Sitta ameeleza kuwa amefanya mazungumzo na viongozi wakuu wa dini ili kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yakifikishwa kwa viongozi hao.

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, akisalimiana na kiongozi wa dini ya Kiislamu nchini Tanzania, Sheikh Mkuu Mufti Shaaban Simba jijini Dar es Salaam jana.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kuonana na kiongozi wa Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo pamoja na Kiongozi wa Waislamu nchini Mufti Sheikh Shaaban bin Simba, Mh. Sitta amesema kutokana na umuhimu wa viongozi hao ameamua kuchukua jukumu la kuwafafanulia juu ya baadhi ya mambo.

Aidha Sitta amesema amewasilisha maombi kwa rais Jakaya Kikwete ya kumtaka kusitisha kwa muda vikao vya bunge hilo ili kutoa muda kwa vikao vya bajeti vya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo vinatarajia kuanza hivi karibuni.

Mbali ya kuomba kuahirishwa kwa vikao vya bunge maalumu la katiba, mheshimiwa Sitta amewaambia waandishi wa habari kuwa amemuomba rais kuongeza muda wa bunge hilo kutoka siku sabini zilizokuwa zimepangwa kisheria.