Monday , 11th Jan , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 11 Januari, 2016 amemtembelea na kumpa pole Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Frederick Sumaye ambaye amelazwa katika Taasisi ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano Ikulu imesema kuwa Mheshimiwa Frederick Sumaye alilazwa katika Taasisi hiyo siku nne zilizopita kwa matibabu ya moyo na madaktari wanaomtibu wamemhakikishia Rais Magufuli kuwa anaendelea vizuri ikilinganishwa na wakati alipofikishwa katika Taasisi hiyo.

Pamoja na kumpa pole, Rais Magufuli pia amemuombea apone haraka ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kuonana na Rais, Waziri Mkuu Mstaafu Sumaye amemshukuru Rais Magufuli kwa kwenda kumuona na kueleza kuwa kitendo hicho kimeonesha jinsi alivyo na upendo wa dhati na anavyowajali watu wake.

Kuhusu hali yake, Mheshimiwa Sumaye amesema anaendelea vizuri, anapata matibabu mazuri na kwamba kwa kuwa hali yake ni nzuri anatarajia kuruhusiwa kuondoka hospitali hapo baada ya muda mfupi.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo imesema kuwa Rais John Magufuli amemtembelea na kumpa pole mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere kufuatia kifo cha Mkwewe Leticia Nyerere kilichotokea jana huko Maryland Marekani alikopelekwa kwa ajili ya kupata matibabu mapema mwezi huu.

Pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli pia amewapa pole wanafamilia wote na amewaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.

Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere Bwana Joseph Butiku amemueleza Rais Magufuli kuwa familia inaendelea na taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani na itatoa taarifa baadaye.