Thursday , 24th Dec , 2015

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limewatahadharisha wananchi juu ya kufanya vitendo vitakavyosabisha uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha sikukuu, na kuahidi kuwachukulia hatua watakaojaribu kufanya hivyo kwani jeshi hilo limeimarisha ulinzi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, ACP Henry Mwaibambe.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Henry Mwaibambe, amesema, wananchi wanatakiwa kuungana na jeshi hilo katika jitihada za kuhakikisha amani inaendelea kutawala na kwamba watakaokwenda kinyume waripotiwe polisi haraka.

Amewataka watumiaji wa barabara hasa wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani na kuacha kuendesha vyombo vyao wakiwa katika hali ya ulevi jambo ambalo linaweza kusababisha ajali kwa kukosa umakini.

Aidha, amewaonya wenye tabia za kutoa taarifa za uongo kwa jeshi hilo, tabia ambazo zimejitokeza hasa kwa mawakala wanaoshughulika na ununuzi wa zao la korosho kwa kudai wameibiwa pesa za kununulia zao hilo jambo ambalo sio la kweli .