Mkuu wa Chuo kikuu Cha Dodoma (UDOM) Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akimtunuku mmoja wa wahitimu.
Mwenyekiti wa bodi ya chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Balozi Augustino Mahiga amewaasa wanafunzi waliohitimu katika chuo hicho kujiongezea elimu ya ufundi na ujuzi mpya katika fani mbalimbali ili kujiongezea fursa za ajira na kupanua wigo wa ujasiriamali.
Balozi Mahiga ametoa kauli hiyo jana kwenye mahafali ya sita ya chuo hicho ambapo amewahusia kuwa ubora wa shahada zao wakati mwingine siyo kielelezo cha ubora katika utendaji na wala siyo mwisho wa elimu na kwamba uelewa wa mambo hupatikana kwa kujiendeleza.
Balozi Mahiga alisema kuwa taifa linawasubiri kwa hamu kubwa kupata mchango wao katika mustakabali wake wa kujenga mazingira yenye rutuba ya uwezeshaji mkubwa zaidi na hivyo kutobweteka na kusubiri kuajiriwa
Aidha alisema wananchi pia wanahitaji kuwezeshwa ili waboreshe hali zao za maisha tu bali ni pamoja na kupata uwezo makini wa utambuzi na ukuzaji wa fursa zilizopo katika kujiendeleza na kusaidia kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
Kwa upande wake makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula amesema jumla ya wahitimu 4,136 wamehitimu katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo vyeti, stashahada, shahada, shahada za uzamili na shahada za uzamivu za chuo Kikuu cha Dodoma.
Naye mkuu wa chuo hicho Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa amejivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa na chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa.