Thursday , 12th Nov , 2015

Tanzania imetajwa kuwa ni nchi pekee duniani inayouza korosho ghafi kwa bei ya juu zaidi kutokana na kuwa na korosho bora na zenye soko zuri kiasi cha kuwafanya wanunuzi kununua kwa bei nzuri.

Wakulima wakipakia Korosho baada ya kutoka kuzivuna Mashambani

Hayo yamezungumzwa leo mkoani Mtwara na mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania, Mfaume Juma, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa msimu wa ununuzi wa korosho ghafi kwa mwaka 2015/2016.

Aidha, amesema bodi inajivunia mafanikio ya kuurejesha mkoa wa Pwani katika ununuzi wa zao hilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao ulikwama toka msimu wa mwaka 2011/2012.

Amesema, miongoni mwa baadhi ya changamoto zinazoikumba bodi kwa sasa ni kutotekelezwa kwa mfumo huo katika wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma kama ilivyopitishwa katika mkutano wa wadau wa Agosti 28 na 29 mwaka huu uliofanyika mkoani Lindi.