
CAF imeliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulielekeza lihakikishe kesi dhidi ya viongozi wa ZFA inafutwa na wanarejeshwa madarakani, vinginevyo Zanzibar itafungiwa katika soka ya kimataifa.
Barua ya CAF kwa TFF imesema kwamba iwapo agizo hilo litakiukwa, Zanzibar itatengwa na nchi zote wanachama wa CAF na FIFA ikiwa na maana kuwa hakuna timu ya nje ya nchi hiyo itakayokwenda kucheza michuano ya kila mwaka ya mapinduzi visiwani humo na Zanzibar haitaruhusiwa kucheza kombe la Challenge wala Kagame.
CAF imesema, klabu za Zanzibar pia mwakani zitapoteza haki ya kucheza michuano ya Afrika, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa.
Mahakama Kuu ya Zanzibar iliwaamuru viongozi wa juu wa ZFA kuondoka madarakani na kuagiza kuundwa kamati ya muda kwa ajili ya kusimamia shughuli za chama hicho.
Rais wa ZFA Ravia Idarous, Makamu wake ofisi ya Pemba Ali Mohammed pamoja na katibu mkuu Kassim Haji Salum, waliambiwa kwa mujibu wa katiba ya ZFA muda wao wa kukaa madarakani umemalizika na hivyo wakae pembeni.
Mahakama pia ilitoa agizo la kuundwa kamati ya muda ya uongozi wa chama hicho ambacho mbali na kesi ya ubadhirifu wa fedha, inakabiliwa na kesi mbili za kukiuka katiba na kanuni za mashindano, zilizofunguliwa dhidi yake na klabu za Chuoni SC na Aluta.
Baada ya amri hiyo ya mahakama, Umoja wa Klabu za Soka Zanzibar uliteua kamati ya watu saba kuandaa uchaguzi mkuu wa chama hicho ili kupata viongozi wapya.
Waliteuliwa ni Hussein Ali Ahmada anayekuwa mwenyekiti ambapo makamu wake atakuwa Omar Ahmed Awadh.
Aidha, Hashim Salum Hashim anakuwa katibu mkuu akisaidiwa na Khamis Hamad, wakati Masoud Attai Masoud, Salum Hamdun na Ali Ussi Jongo wanakuwa wajumbe wa kamati hiyo.
Jongo alisema miongoni mwa majukumu makubwa ya kamati hiyo ni kuzungumza na uongozi wa klabu za Chuoni SC na Aluta, kuziomba ziondoshe kesi walizofungulia ZFA ili mpira uchezwe na ligi zianze.
Jongo amesema kazi nyengine ni kuandaa utaratibu wa kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho ambacho kwa muda sasa shughuli zake zimekwama kutokana na kuelemewa na mzigo wa kesi mahakamani.