Mgombea wa ACT-Wazalendo jimbo la Njombe Kusini, Emilian Msigwa akiongea na Wanakijiji cha Ihanga
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe Mgombea huyo amelalamika kuhusiana na vurugu hizo leo akisema kuwa zilitokea juzi katika mkutano wake uliokuwa ukifanyika katika kijiji cha Yakobi cha jimbo hilo.
Msigwa amesema kuwa katika kata ya Yakobi amekuwa akipata shida ya kufanya kampeni katika vijiji vyake kutokana mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia CCM kuweka vikwazo vya kuzuia mikutano ya chama hicho kwa kuweka ratiba zake na kufanya hujuma na watendaji wa vijiji hivyo.
Akizungumzia ulinzi wa polisi katika mikutano yao alisema kuwa katika mikutano yao mingi ya vijiji huwa wanaenda bila ya kuwa na polisi kutokana na umbali wa maeneo na kuwa na imani ya kuwa na amani katika maeneo hayo na kusema kuwa mikutano ya mjini huwa wanakuwa na polisi.
Msigwa ameongeza kuwa ameshiriki chaguzi nyingi lakini hajawahi kuona CCM wanafanya vurugu kama vyama vingine lakini mwaka huu ni tofauti na kuwa CCM wamebanwa.
Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Wallboard Mtafungwa, amesema kuwa tukio hilo limewafikia na kuwa wanamshikilia Erasto Ngole (43), mkazi wa Itulike mkoani humo mwanachama wa CCM na wengine saba wanatafutwa kuhusiana na tukio hilo.