Monday , 28th Sep , 2015

Mlipuko wa Kipindupindu umeibuka tena katika kata ya mindu manispaa ya Morogoro baada ya mtu mmoja kufariki nyumbani kwake na kuzua hofu kubwa kwa wakazi wa manispaa hiyo.

Afisa Afya manispaa ya Morogoro Gabriel Malisa

Akizungumza katika kambi maalumu ya wagonjwa wa kipindupindu Afisa Afya manispaa ya Morogoro Gabriel Malisa amemtaja aliyefariki kuwa ni Mkolole Shomari (65).

Amesema mtu huyo amefariki dunia nyumbani kwake muda mfupi baada ya majirani zake mama na mtoto waliotokea jijini Dar es Salam wakiwa na ugonjwa huo na baadaye kutibiwa ndipo marehemu alianza kuugua ugonjwa huo bila kuchukua tahadhari hatimaye kupoteza maisha.

Hata hivyo malisa amesema kwa zaidi ya siku 14 zilizopita hakukuwa na mgonjwa yeyote aliyeripotiwa kuwa na dalili za kipindupindu ndani ya manispaa ambapo amewataka wananchi wa mkoa wa huo na mikoa jirani kuchukua tahadhari mapema wanapopata wageni kutoka jijini Dar es Salaamu pamoja na kuimarisha hali ya usafi wa mazingira na vyakula ili kutokomeza kabisa mlipuko huo.

Nao wakazi wa mji wa Morogoro wamewataka wanasiasa kutumia majukwaa ya mikutano ya kampeni kuhamasisha wananchi kujikinga na mlipuko huo wa kipindupindu kwani wanaoathirika na mlipuko huo ni miongoni mwa wapigakura wao.