Wednesday , 12th Aug , 2015

Serikali ya Tanzania imesema imeanza mchakato na juhudi za kidiplomasia ili kuachiwa huru kwa Masheikh wa Tanzania waliotekwa nyara Kivu ya Kaskazini nchini Congo karibu wiki moja iliyopita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Mindi Kasiga.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Mindi Kasiga amesema kuwa serikali ilipata taarifa hizo kupitia balozi za Tanzania nchini humo na kuthibitishwa ni kweli Masheikh hao waliotekwa nyara ni Watanzania.

Bi. Mindi amesema kuwa baada ya serikali kuthibitisha kuwa Masheikh hao ni Watanzania Serikali inafanya kila linalowezekana ili kuwakomboa na kuwarudisha nchini Salama na kwa hiyo kila taarifa kuhusu watu hao wanaipa umuhimu.

Aidha ameongeza kuwa mpaka sasa haijajulikana na kikundi gani kimehusika na utekeaji huo kwa kuwa nchini humo kuna vikundi mbalimbali vyenye silaha ambavyo hujipatia pesa kwa njia yoyote lakini mpaka sasa Serikali haijapata taarifa ya kiasi gani watu hao wanahitaji kupatiwa.