Monday , 10th Aug , 2015

Serikali imepanga kurejesha mpango wa utoaji pembejeo za ruzuku kwa wakulima wadogo nchini uliositishwa kwa msimu mmoja uliopita ili kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo na kuwafanya wakulima kufaidika na ukuaji wa uchumi wa nchi unaotajwa kukua.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kitazama mkungu wa Ndizi uliletwa katika maonyesho ya nanenane Mbeya na Bosco Luambano (kulia) wa Kijiji cha Hanga

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda ametangaza mpango huo jijini Mbeya wakati akifunga maonyesho ya kilimo ya nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale na kusema hali itakayosaidia wananchi wengi kuondokana na umaskini wa kipato kwa kukuza pato la taifa na la mtu mmoja mmoja

Pinda ameongeza licha ya viashiria vya ukuaji wa uchumi kuonesha kuwa Tanzania inaelekea kuondoka kwenye kundi la nchi maskini ifikapo mwaka 2025 bado wananchi wake ni maskini kutokana na uchumi huo kubebwa na sekta ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na wananchi wa kawaida.

Wakati huo huo Pinda amesema maonyesho ya siku ya wakulima nchini maarufu kama Nane Nane ni sawa na shamba darasa ambalo washiriki na wananchi wanapata fursa kujifunza mambo mapya kila mwaka.

“Maonyesho ya Nane Nane ni shamba darasa kubwa, nimetembelea mabanda mengi na kubaini kuwa sasa hivi kuna fikra mpya ambazo hazikuwepo wakati wa maonyesho ya mwaka jana,” alisema.

“Maonyesho haya yana umuhimu mkubwa kwani yanatoa fursa kwa wananchi wanaokuja uwanjani kupata ujuzi na maarifa mapya ili waone kwa namna gani wanaweza kuboresha uzalishaji wa mazao au mifugo yao,” aliongeza.

Aliwataka viongozi wa Jumuiya ya Wakulima Tanzania (TASO) ambao ni waandaaji wa maonyesho hayo, wabadili mtazamo wao na mwakani (2016) waweke utaratibu wa kufanya tathmini ya maonyesho hayo kwa kuwahusisha zaidi wakulima na kuwapa nafasi ya kuelezea jinsi walivyonufaika na maonyesho hayo.

Aliwataka pia Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa wanaoshiriki maonyesho hayo nao pia wapewe fursa ya kuelezea jinsi walivyonufaika na maonyesho na kwa kiasi wamesaidia kuwapelekea wananchi wanaowaongoza ujuzi na maarifa hayo.

“Mnapaswa mjiulize ni kwa kiasi gani mmewasaidia wakulima na wafugaji huko vijijini kutumia teknolojia mnazozipata huku kwenye maonyesho. Kama viongozi mnapaswa muwapelee elimu ya kubadili maisha ya mvuvi, mkulima au mfugaji, bila kufanya hivyo, sisi tutabakia kuwa wakubwa tu na hatutasawasaidia wanachi wetu,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema hawezi kuhama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka waliohama baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais, wajiulize iwapo wataihama nchi wakishindwa kufanikisha malengo yao huko walikohamia.

“Tulijitokeza wengi kuchukua fomu, watatu wakashindwa kurejesha fomu, wakawa wamejitoa wenyewe. Tulibaki 38 tuliorejesha fomu na kati ya hao wapo waliopita na wengine wakawekwa pembeni. Mimi pia nikawekwa pembeni. Ninaamini kazi tuliyokwenda kuifanya tumeifanya vizuri, tena vizuri sana”.

“Sasa hapa katikati nilikaa kimya kidogo, watu wakaanza kusema kwenye mitandao… Oooh mbona mzee yuko kimya! Au naye anataka kuhamia kule. Sasa niseme nimeachwa huku kwa hiyo nifanyaje? Nihame niende wapi? Hivi, ukihama huku huko unakohamia ukishindwa utahamia wapi tena? Au ndiyo utahama nchi?” alihoji huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu alisema CCM ina Ilani yenye sera nzuri, na ndicho chama kinachopaswa kuaminiwa na Watanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuongeza kuwa anayo imani na sera ya CCM, hana mashaka kuwa chama hicho kitapata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Waziri Mkuu aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa jitihada zake katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, ikiwemo uandikishaji wapigakura ambao wamevuka malengo yaliyowekwa awali.

“Licha ya changamoto nyingi zilizoibuka tangu kuanza kwa uandikishaji wapiga kura nchini kupitia mashine za Biometric Voters Register (BVR), Tume imeandikisha zaidi ya wapiga kura milioni 24 na imevuka malengo yaliyowekwa awali ya kuandikisha watu milioni 22,” alisema.