Kushoto kiungo mshambuliaji wa Simba Awadh Juma akishangilia goli lake akiwa na kiungo wa pembeni Simon Sserunkuma.
BAO pekee la Awadh Juma Issa dakika ya 89, limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya SC Villa ya Uganda katika mchezo wa kirafiki jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kuhitimisha tamasha la Simba Day, Awadh alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliorudi kufuatia kupanguliwa na kipa Stephen Odongo baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa SC Villa.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Simba SC, kwani SC Villa walionekana kuwa wapinzani wagumu kwao tangu mwanzo, licha ya kucheza pungufu tangu dakika ya 44 baada ya Yoseri Waibi kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Ibrahim Hajib.
Simba SC ilianza kucheza soka ya kuvutia na kusisimua mashabiki wake kipindi cha pili, baada ya kocha Muingereza Dylan Kerr kufanya mabadiliko kadhaa na hivyo kuanza kufufua matumaini ya mashabiki wa timu hiyo kuona timu yao ikipata ushindi kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa tamasha hilo kwani ilikuwa ikipoteza michezo yake yote katika matamasha yote ya siku ya Simba yaliyopita.
Waliobadili mchezo ni beki anayemudu kucheza upande wa kulia na kushoto, Mrundi Emery Nimubona ambaye alikuwa anatia krosi maridadi zilizozua kizazaa langoni mwa wapinzani na Mwinyi Kazimoto ambaye alikwenda kuiongoza timu vizuri katika idara ya kiungo ambayo awali ilionekana kucheza vema lakini bila mipango ya ushindi.
Kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast ambaye yuko katika majaribio yakusaka nafasi ya kusajiliwa na timu hiyo hii leo alikuwa kivutio kikubwa kwea mashabiki wa Simba kutokana na kulinda vizuri lango lake, ikiwa ni pamoja na kuokoa michomo kadhaa ya hatari iliyoelekezwa langoni mwa Simba na washambuliaji hatari wenye uchu wa magoli wa klabu ya Villa maarufu kama Jogoo kule Kampala.
Mshambuliaji Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyewahi kucheza kwa mahasimu wa Simba, Yanga SC alikuwa mwiba kwa mabeki wa SC Villa, lakini alishindwa kuzifumania nyavu za wapinzani wao hao.
Pamoja na ushindi huo, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, kocha Kerr ana kazi nzito ya kufanya ili Simba SC ifikie katika ubora wa kuweza kushindania taji dhidi ya timu za Azam FC na Yanga SC ambazo zimefanya usajili wa kutisha msimu huu.
Mchezo pamoja na mchezo huo na burudani nyingine zilizokuwepo hii leo kivutio kikubwa katika tamasha hilo kilikua ni mchezo baina ya viongozi wa timu ya Simba na timu ya kombaini ya wasanii wa bongo Fleva na Bongo Muvi na viongozi wa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwa goli safi lililofungwa na kocha mkuu wa timu hiyo mwingereza Dylan Kerr.
Ikumbukwe hilo ni tamasha kubwa la kila mwaka Siku ya Simba maarufu kama Simba day ambalo kilele chake huwa kila ifikapo tarehe nane mwezi wa nane kila mwaka