Thursday , 30th Jul , 2015

Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Edward Lowassa amechukua fomu ya kuwania urais kwa tiketi ya chama cha siasa cha upinzani Chadema na kuahidi kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utashinda urais katika uchaguzi mkuu.

Mbunge wa Monduli Edward Lowassa akionesha fomu ya kugombea urais mara baada ya kukabidhiwa leo.

Mhe. Lowassa ametoa ahadi hiyo leo Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya ofisi za Chadema Kinondoni, mara baada ya kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuwania urais kwa kupitia chama hicho.

Ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika zoezi linaloendelea ili kuufanya ushindi huo wa urais kuwa wa kura nyingi sana.

Hii ni mara ya pili kwa Mh. Lowassa kuchukua fomu za kuwania urais, ambapo awali alichukua fomu za urais kupitia chama tawala cha CCM, lakini jina lake likakatwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM jambo lililopelekea kuhamia katika chama cha Chadema.