Tuesday , 28th Jul , 2015

Hiyo inafuatia Gor Mahia inayofundishwa na Mscotland, Frank Nutal kuifunga mabao 2-1 Malakia ya S

Gor Mahia ya Kenya itamenyana na Khartoum N ya Sudan katika Nusu Fainali ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Ijumaa wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hiyo inafuatia Gor Mahia inayofundishwa na Mscotland, Frank Nutal kuifunga mabao 2-1 Malakia ya Sudan Kusini katika Robo Fainali ya pili jioni hii Uwanja wa Taifa, Jijini.

Shujaa wa Gor Mahia leo alikuwa mchezaji wa kimataifa wa Uganda, Godfrey Walusimbi aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha kwanza dakika za tatu na 28, yote kwa kazi nzuri ya Michael Olunga.
Bao pekee la Malakia lilifungwa na Thomas Jacob dakika ya 64 na baada ya hapo, Gor Mahia wakaanza kucheza kwa kujihami zaidi kuhofia kuruhusu bao la kusawazisha.

Robo Fainali ya kwanza, Khartoum N, washindi hao wa tatu wa Kundi A, nyuma ya Yanga SC na Gor Mahia, waliifunga APR ya Rwanda mabao 4-0 Uwanja wa Taifa.

Mabao ya Khartoum N inayofundishwa kocha Mghana, Kwesi Appiah yalifungwa na Atif Khali dakika ya 10, Amin Ibrahim dakika ya 19 na 36 na Salah Eldin Osman dakika ya 81. Ikumbukwe Gor Mahia na Khartoum zilikutana awali na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Kundi A.

Robo Fainali nyingine zitachezwa kesho kati ya Al Shandy Sudan dhidi ya KCCA ya Uganda kuanzia Saa 7:45 mchana na baadaye Azam FC dhidi ya Yanga SC, Uwanja huo huo wa Taifa, Dar es Salaam.

Nusu Fainali zitafuatia Ijumaa na Fainali pamoja na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu itakuwa Jumapili, siku ya kilele cha mashindano hayo.